Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amemrudisha kwenye kikosi cha Ligi ya Mabingwa Ulaya, kiungo wake Yaya Toure.

Toure ambaye aliachwa kwenye kikosi cha wachezaji 25 kwenye hatua ya makundi ya Ligi hiyo baada ya wakala wake, Dimitri Seluk kutoa maneno ya kejeli kwa Guardiola amerudishwa kufuatia uwezo mkubwa anaouonyesha kwenye mechi za ligi kuu ya Uingereza.

Tangu kuumia kwa kiungo wa Ujerumani, Ilkay Gundogan, Toure amefanikiwa kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi hicho.

Guardiola pia amemjumuisha mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Gabriel Jesus kwenye nafasi ya Kelechi Iheanacho, ambaye hata hivyo bado anaruhusiwa kurejeshwa kwenye kikosi cha michuano hiyo.

City watakutana na mabingwa wa zamani wa ligi ya Ufaransa, Monaco kwenye hatua ya 16 bora ambapo mechi ya kwanza itachezwa tarehe 21 mwezi huu.

Toure alilazimika kumuomba radhi hadharani Pep Guardiola ambaye aliapa kutompa nafasi kiungo huyo mpaka wamalize tofauti zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *