Mfanyabiashara nchini, Ndama Shaaban Hussein ‘Pedeshee Ndama Mutoto ya Ng’ombe’ jana amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kosa la utapeli wa dola za Kimarekani 540, 390 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 1.17.

Ndama amesomewa mashtaka sita mbele ya Hakimu Victoria Nongwa na Mwendesha Mashtaka Leonard Msigwa akisaidiana na Christopher Challo kuwa, mnamo Februari 20, 2014 mkoani Dar, Ndama alitengeneza nyaraka feki, zikionesha kupata kibali cha kusafirisha sampuli za madini ya dhahabu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Shtaka la pili, tatu na nne pia yalikuwa ya kugushi nyaraka, ikiwemo iliyotoka Umoja wa Mataifa, iliyoisafisha kampuni yake ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Ltd kuwa imeruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu.

Nyaraka hizo zililenga kuiaminisha Kampuni ya Trade TJL DTYL Ltd ya Australia kuwa Muru ni Kampuni halali kwa biashara hiyo. Pia Ndama alidaiwa kugushi nyaraka zilizoonesha kuwa alilipa kiasi cha dola 331, 200 sawa na shilingi milioni 728 kwa TRA kama kodi ya kupitisha mzigo huo hapa nchini.

Shtaka la tano la Ndama ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kiasi cha dola 540,390 (sawa na shilingi bilioni 1.177) kutoka kampuni hiyo ya Australia zilizowekwa katika akaunti ya Kampuni ya Muru katika Benki ya Stanbic na shtaka la sita lilihusu kosa la utakatishaji fedha hizo.

Ndama amekana mashtaka yote na kesi yake imeahirishwa hadi Desemba 13, mwaka huu itakapotajwa tena.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *