Mfanyabiashara maarufu nchini, Shabani Hussein ‘Ndama Mtoto wa Ng’ombe’ anayekabiliwa na mashtaka sita katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu amekiri mashitaka ya kutakatisha fedha ambazo ni Dola za Marekani 540,000 (Sh bilioni 1.208).

Hiyo ni zaidi ya mara tatu kwa Hussein kukiri kosa hilo anaposomewa mashitaka yake na inapofika hatua ya kusomewa maelezo ya awali, anakana mashitaka hayo.

Wakili wa Serikali, Estazia Wilson alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa hata hivyo, mshitakiwa aliomba mahakama hiyo kumkumbushia mashitaka yake ambapo kwa mara nyingine alikiri kosa la sita la utakatishaji fedha.

Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa wiki hii kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kutakatisha Fedha, Kifungu cha 12(a)na 13(1)(a) Namba 12 cha 2016, Mshitakiwa huyo anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka isiyopungua mitano ama isiyozidi 10 ama kulipa faini isiyopungua Sh milioni 100 ama isiyozidi Sh milioni 500.

Katika mashitaka hayo, anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014, Dar es Salaam, akiwa Mwenyekiti na mtia saini pekee wa Kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye Benki ya Stanbic alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa Dola za Marekani 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la kujiapatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Licha ya kukubali mashitaka hayo, Ndama alikana makosa mengine yakiwemo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *