Mfanyabiashara nchini, Ndama Shabani Hussein, maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto ya Ng’ombe amepata dhamana baada ya kulipa milioni 200.

Ndama amepata dhamana baada ya kuwa na wadhamini wawili na kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani zaidi ya shilingi milioni 600.

Wiki iliyopita Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimtia hatiani Ndama na kumuhukumu kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya milioni 200 baada ya kukiri shtaka la kutakatisha USD 540,000.

Aidha mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa ilimsomea masharti ya dhamana mshtakiwa huyo iwapo angefanikiwa kulipa kiasi hicho cha milioni 200 ili awe huru katika mashtaka matano yanayoendelea kumkabili mahakamani hapo ambayo upelelezi wake bado haujakamilika.

Katika masharti hayo, Ndama alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na atoe fedha taslimu kiasi cha USD 270,200 ambacho ni sawa na zaidi ya milioni 600 mahakamani hapo ama mali isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha

Licha ya kupata dhamana, Ndama alirudishwa gerezani kukamilisha taratibu kabla ya kuachiwa huru.

Hukumu hiyo ya shtaka la sita la kutakatisha fedha ilitolewa baada ya Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa kumsomea maelezo ya awali (PH) Ndama na kuyakubali maelezo ya awali na maelezo yote yanayounda shtaka hilo la kutakatisha fedha, akapatikana na hatiani na kupewa adhabu hiyo.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili Msigwa aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa amekubali shtaka la sita la kutakatisha fedha na maelezo yanayounda shtaka hilo, hawana kumbukumbu za nyuma za makosa dhidi ya Ndama ila ni rai ya upande wa mashtaka kuwa wakati mahakama ikitoa adhabu izingatie matakwa ya kifungu cha 13(a) cha sheria ya kuzuia utakatishaji fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *