Mtoto aliyetambuliwa kwa jina la Isack Ernest (16) anayetuhumiwa kuwa miongoni mwa vijana wa kikundi cha uhalifu cha ‘panya road’ amezinduka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Ernest, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Lumo na mkazi wa Buza, anayedaiwa kuwa miongoni mwa vijana wa kikundi hicho, alidhaniwa amekufa baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kwa tuhuma za kuwaibia mali zao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Gilles Muroto amesema walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna vijana watatu wamekufa katika eneo la Mbagala na baada ya kufika eneo la tukio waliwakuta vijana hao wakiwa na hali mbaya.

Kamanda Muroto alimtaja mmoja aliyejulikana kwa jina la Kelvin Nyambocha (14) kuwa alikufa baada ya kupigwa na kuchomwa moto na wananchi na kwamba kabla ya mauti kumkuta alifuatana na wenzake kwa ajili ya kwenda kuangalia tamasha la muziki wa Singeli lililofanyika Mbagala Zakhem.

Kijana mwingine Selemani Hamis (16), mkazi wa Kilingule, alifariki akiwa chumba cha upasuaji katika hospitali ya wilaya Temeke.

Amefafanua kuwa Ernest alipigwa hadi kuzimia na wananchi hao walijua kuwa amekufa ambapo alipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na kufanyiwa taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa nguo kuwekewa namba na kuingizwa kwenye jokofu.

Kamishna Muroto amesema baada ya kupata fahamu na afya yake kutengemaa alihojiwa na kuwataja wenzake 10 ambao yuko nao katika kundi moja.

Amesema kijana mwingine fundi magari aitwaye Faraji Suleiman (19) mkazi wa Buza Kwa Rulenge, hali yake ni mbaya na amelazwa katika Hopitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *