Msajili wa Vyama ya Siasa, Jaji Francis Mutungi ametoa orodha ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na viongozi wa vyama hivyo ambako inasisitiza kuwa Profesa Ibrahim Lipumba ndiye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na Katibu Mkuu ni Seif Shariff Hamad.

Kwa mujibu wa barua hiyo ya Oktoba 4 mwaka hu iliyoandikwa kwenda kwa makatibu wakuu wa vyama vyenye usajili wa kudumu, Profesa Lipumba ambaye Baraza Kuu la chama hicho limetangaza kumfukuza uanachama, anaonekana kwenye orodha hiyo kama Mwenyekiti wa CUF.

Jina la Profesa Lipumba ambaye alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo mwaka jana, limerejeshwa kwenye orodha na Msajili wa Vyama ya Siasa baada ya yeye mwenyewe kutangaza kutengua barua yake ya kujiuzulu.

Kwa hatua hiyo ya Msajili, uteuzi wa Julius Mtatiro ambao umefanywa na Baraza Kuu kuongoza Kamati ya Uongozi ya CUF hautambuliwi na Ofisi ya Msajili wa Vyama ya Siasa.

Uamuzi huo wa Ofisi ya Msajili umekuwa unalalamikiwa na upande unaoongozwa na Maalim Seif kuwa unakiuka Katiba ya CUF wakati yeye akisisitiza kuwa yuko sahihi kumtambua Profesa Lipumba kwa mujibu wa Katiba hiyo.

Barua hiyo imevitaja vyama 22 ambayo vina usajili wa kudumu na chama cha mwisho kusajiliwa ni Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) ambacho viongozi wake ni Anna Mghwira ambaye ni Mwenyekiti na Katibu Mkuu ni Juma Sanani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *