Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema kuwa kwasasa nguvu kubwa itaelekezwa kwa watoto watatu wa Shule ya Lucky Vicent ambao wanapatiwa matibabu nchini Marekani.
Gambo aliyasema hayo katika taarifa yake kupitia vyombo vya habari aliyoitoa jana kuwa hivi karibuni, ofisi yake ilitoa taarifa ya mapato na matumizi kuhusu michango ya rambirambi ya ajali ya basi ya shule ya Lucky Vincent iliyotokea Wilayani Karatu eneo la Rhotia.
Amesema ajali hiyo ilipotezea watu 35, wakiwemo wanafunzi 32, walimu 2 na dereva 1. Aidha, ajali hiyo pia ilibakiza majeruhi 3 ambao ni Wilson Tarimo, Sadya Awadh na Doren Elibariki.
Gambo amesema baada ya serikali na wadau mbalimbali nchini kushirikiana kufanikisha kuihifadhi miili, ikiwa ni pamoja na kutoa rambirambi ya Sh 3,857,000 kwa kila familia iliyofiwa.
Amesema hivi sasa wameona ni vema nguvu kubwa ikaelekezwa kwenye kuwahudumia majeruhi ili waweze kupona na makusudio ya Mungu yaweze kutimia.
Mkuu wa mkao huyo amesisitiza kuwa anapenda kuujulisha umma kuwa leo, atatuma kwa familia za majeruhi pamoja na madaktari waliojitoa kuwasindikiza majeruhi kiasi cha Dola za Marekani 20,000, sawa na Sh 44,720,000 za kitanzania.
Kwa ujumla baada ya yote hayo kutabakiwa na kiasi cha Sh 23,273,885 huku wakiendelea kuangalia hali za majeruhi. Kiasi cha fedha kilichobaki kitaendelea kuwekewa utaratibu kupitia timu ya wafiwa 4 walioteuliwa na wafiwa wenzao kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha mapato na matumizi ya suala hili yanaeleweka vema kwa umma.
Pia ametoa rai kwa wananchi kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha imehitimisha rasmi suala zima la kupokea rambirambi ili ipate muda zaidi wa kufuatilia mustakabali wa majeruhi walioko haspitalini nchini Marekani.