Rais wa Marekani, Barack Obama amemwalika Rais mteule wa nchi hiyo Donald Trump Ikulu ya White House kwa ajili ya kufanya mkutano wa pamoja.

Rais Obama amesema lengo la mkutano wao itakuwa kujadiliana kuhusu shughuli ya mpito na kupokezana madaraka.

Trump wa chama cha Republican atakuwa rais wa 45 wa Marekani baada ya kupata ushindi wa kushangaza dhidi ya Hillary Clinton wa chama cha Democratic siku ya jumanne.

Obama alifanya kampeni kali kumzuia Trump kushinda huku akisema hafai kuongoza nchi hiyo kutoakana na sera zake za kibaguzi.

Lakini rais Obama amewahimiza Wamarekani wote kukubali matokeo ya uchaguzi wa Jumanne na kushirikiana na Trump.

Licha ya Rais Obama kuhimiza umoja na Bi Clinton kuwaambia wafuasi wake kwamba Trump anafaa kupewa nafasi ya kuongoza ushindi wake umezua maandamano katika miji na majimbo kadha Marekani.

Mamia ya waandamanaji wanaompinga Trump walikusanyika nje ya jumba kuu la Bw Trump, Trump Tower eneo la Manhattan jijini New York jana Jumatano wakibeba mabango yaliyokuwa na ujumbe “Not my president” .

Polisi hapo awali waliweka vizuizi vya saruji pamoja na kuchukua hatua nyingine za kiusalama nje ya jumba hilo refu linalopatikana barabara ya 5th Avenue, jumba ambalo huenda likawa makao makuu ya Trump wakati wa kipindi cha mpito kabla yake kuingia White House

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *