Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ina mpango wa kurejesha nyumba 71 zilizouzwa kwa wafanyakazi bila kufuata utaratibu.

Taasisi hiyo imetoa siku 60 kwa wafanyakazi 457 ambao hawakulipa au wamefanya malipo kidogo kukamilisha malipo, kinyume chake watanyang’anywa nyumba zao.

Meneja Mkuu wa Tazara (Tanzania), Fuad Abdallah alitoa maagizo hayo jana alipotembelea baadhi ya nyumba zilizouzwa katika vituo vya Vigama na Kifuru.

Amesema hatua ya kurejesha nyumba hizo imelenga kunusuru nyumba 71 ambazo ziliuzwa baada ya muda wa mwisho uliowekwa wa mwaka 2008 huku nyumba nyingine 19 ambazo uuzwaji wake ulikuwa na utata jambo ambalo limefanya shirika hilo kufungua kesi mahakamani.

Amesema baada ya kufanya ukaguzi, Mamlaka imebaini kuwa baadhi ya nyumba zinazomilikiwa na ama wafanyakazi au wastaafu, baadhi ya watu walioorodheshwa kama wamiliki walikana kumiliki au kununua nyumba hizo.

Meneja huyo amesema nyumba zilizo sambamba na reli ya Tazara kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduma, ni nyumba 831 zilizouzwa kihalali na nyumba 774 zimebaki kwenye taasisi ambazo zinatumika na wafanyakazi katika vituo mbalimbali.

Amesema kazi ya uuzaji wa nyumba hizo ulifanyika kati ya mwaka 2002 hadi 2008 baada ya Bodi ya Wakurugenzi kutoa kibali cha uuzaji mwaka 1999 lengo likiwa ni kupunguza gharama za uendeshaji na matengenezo ya nyumba hizo.

Kwa mujibu wa Abdallah, wamiliki wa nyumba 201 hawajalipa malipo yoyote ambapo Mamlaka ilitarajia kukusanya Sh milioni 178 huku wamiliki wengine 256 wamelipa kidogo na wanatarajia kukusanya Sh milioni 192 watakapomalizia madeni yao.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *