Afrika bado inaendelea kutafakaria juu ya hatua itakayofuata ya Mkuu wa zamani wa Tume ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma.

Akiwa na uzoefu mkubwa unaotokana na miaka zaidi ya ishirini ya utumishi huku akiwa na ushawishi mkubwa na nguvu ya kisiasa tangu alipokuwa waziri nchini kwake Afrika Kusini hadi wakati alipokuwa mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika, na sasa baada ya kustaafu nafasi hiyo, Dlamini-Zuma anatarajiwa kugeukia siasa za ndani nchini Afrika Kusini.

Dlamini-Zuma mwenye miaka 67, amewahi kuwa waziri kwenye vipindi vyote vinne vya marais walioongoza nchi hiyo baada ya utawala wa kibaguzi.

Amewahi kushika nyadhifa za uwaziri kwenye wizara mbalimbali tangu mwaka 1994 ambapo amewahi kuwa waziri wa afya, mambo ya nje na mambo ya ndani.

Baada ya kukaa nje ya siasa ya Afrika Kusini kwa takribani miaka minne na kuongoza tume ya Umoja Afrika nchini Ethiopia, sasa Dlamini-Zuma anatarajiwa kuwania uongozi wa chama chake cha ANC na endapo atafanikiwa kutwaa nafasi ya ukuu wa chama hicho ni wazi atapewa nafasi ya kuwania urais wa Afrika Kusini kwenye uchaguzi wa 2019.

Je, atathubutu kumharibia mtalakiwa wake, rais Jacob Zuma?

Nkosazana Dlamini Zuma kwa ufupi:

  • Mwanaharakati wa haki za weusi wakati wa utawala wa kibaguzi
  • Alikimbia Afrika Kusini na kumalizia masomo yake ya udaktari nchini Uingereza
  • Alikutana na matalikiwa wake, rais Jacob Zuma wakati alipokuwa daktari nchini Swaziland
  • Ameishi kwenye ndoa na Zuma kwa miaka 16, mwaka 1998 wakaachana
  • Alikataa kuchukua nafasi ya Makamu wa rais iliyokuwa wazi baada ya Jacob Zuma kutimuliwa kazi mwaka 2007
  • Alikuwa Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika 2012 – 2016

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *