Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) itaanza kutoa Vitambulisho vipya vya Taifa vyenye saini kwa wananchi wote waliokamilisha taratibu za usajili na utambuzi na kuchukuliwa alama za kibaiolojia (Alama za vidole, Picha, Saini ya Kielektroniki).

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Bw. Andrew Massawe; utekelezaji wa zoezi hilo utaanza rasmi Jumatano tarehe 14 Septemba 2016 katika ofisi zote za NIDA zikiwemo ofisi za Wilaya zilizoanza usajili Tanzania Zanzibar na mikoa ya Dar-es-salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, na Ruvuma) pamoja na waheshimiwa Wabunge Dodoma.

Waombaji wote ambao Vitambulisho vyao viko tayari watatumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) katika simu zao za kiganjani (mkononi) kufahamishwa kufika katika vituo vya Usajili kuchukua Vitambulisho vyao.

Amesema kutokana na uwepo wa njia nyingi na salama za kusoma taarifa za mwombaji zilizomo ndani ya kifaa maalumu kilichofichwa kwenye kadi ya mtumiaji (chip); ndiyo maana vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika katika huduma mbalimbali zinazohitaji kumtambua mtumiaji kabla ya kupata huduma.

Akizungumzia wananchi ambao hawakuwahi kusajiliwa, Bw. Massawe amesisitiza kwamba wananchi wote ambao hawakuwahi kusajiliwa na wana umri wa miaka 18 na kuendelea; kwa mikoa ambayo tayari kuna ofisi za usajili, kuendelea kujitokeza kwa wingi kusajiliwa ili kupata Vitambulisho vya Taifa kwani zoezi la usajili ni endelevu.

Wananchi wanakumbushwa kutunza vizuri Vitambulisho vyao ili kuepuka gharama kwani kitambulisho cha Taifa kwa mara ya kwanza kitatolewa bure na iwapo kitapotea, ili kupata kingine lazima mtumiaji akilipie.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *