Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai ametangaza kuunda kamati itakayochunguza biashara ya kusafirisha nje ya nchi ‘mchanga wa dhahabu’ unaofanywa na wawekezaji wa mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagi.

Akizungumza baada ya kutembelea makontena zaidi ya 260 yaliyozuiwa Bandari ya Dar es Salaam, Ndugai alisema Bunge litaunda kamati hiyo na ataitangaza hivi karibuni katika Mkutano wa Bajeti uliopangwa kuanza Aprili 4, mwaka huu.

Amesema wamelazimika kuunda kamati hiyo kutokana na utata uliopo katika biashara hiyo ya makinikia ya shaba maarufu kama mchanga wa dhahabu.

Amesema Watanzania wanahitaji kujua biashara hiyo ya mchanga wa dhahabu inafanywa vipi, nani wanafaidika na biashara hiyo ambayo usafirishaji wake nje ya nchi ulianza tangu mwaka 1998.

Pia asema licha ya kuchunguza biashara hiyo, kamati pia itafanya uchunguzi juu ya uwekezaji wote wa madini na namna Watanzania wanavyofaidika.

Amesema kuita mchanga wa dhahabu ni kupotosha, kwani mchanga huo una madini ya dhahabu, shaba na fedha.

Aidha amesema kwa mujibu wa wataalamu, dhahabu ni kidogo kwenye mchanga huo, lakini akasema kama ni kidogo kwa nini wawekezaji wanapeleka maelfu ya makontena nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *