Aliyekuwa mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumanne mkoani Kilimanjaro.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa amesema kuwa Ndesamburo atazikwa katika makaburi ya familia nyumbani kwake eneo la Mbokomu Wilayani Moshi.

Mwili wake utaagwa katika viwanja vya mashujaa mjini Moshi ambapo viongozi mbali mbali watapata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho.

Pia kutakuwa na salamu kutoka kwa viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, viongozi wa dini na wawakilishi wa makundi mbalimbali ambao watahudhuria mazishi hayo.

Golugwa amesema msiba wa Ndesamburo umewagusa wengi nchini kutokana na mchango wake katika kukuza misingi ya demokrasia ya vyama vingi na kuchangia ustawi wa sekta ya utalii.

Philemon Ndesamburo amefariki juzi katika hospitali ya rufaa ya KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo aliugua ghafla.

Kutokana na msiba huo Chadema wameamuru bendera kupepea nusu mlingoti mpaka maziko ya mwanasiasa huyo yatakapomalizika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *