Mgombea mwenza wa chama cha Republican katika uchaguzi mkuu nchini Marekani, Mike Pence amenusurika kifo baada ya ndege iliyombeba kupata ajali uwanja wa ndege.

Ndege hiyo iliteleza na kuvuka barabara inayotumiwa na ndege kupaa na kutua katika uwanja wa La Guardia jijini New York.

Gavana huyo wa Indiana amewaambia wanahabari kwamba yuko salama baada ya kisa hicho na wala hakuna aliyejeruhiwa.

Bw Pence na abiria wengine takriban 30 waliokolewa kupitia mlango wa dharura wa ndege upande wa nyuma.

Kanda za video za runinga zimemuonesha Bw Pence baadaye akiwa amesimama kwenye mvua karbu na magari ya huduma za dharura akizungumza na baadhi ya maafisa.

Kutokana na ajali hiyo Bw Pence ameahirisha hafla ya kuchangisha pesa ambayo ilifaa kuandaliwa katika jumba la Trump Tower eneo la Manhattan, na akaelekea moja kwa moja hadi hotelini.

Kwa upande wake mgombea urais wa chama cha Republican, Donald Trump alimpigia simu Bw Pence kumjulia hali baada ya kisa hicho.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *