Ndege iliyowabeba wanafunzi watatu majeruhi imewasili salama leo majira ya asubuhi nchini Marekani.

Hayo yamebainishwa na mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyarandu ambaye alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha safari hiyo inafanikiwa na watoto hao wanasafirishwa kwenda nchini Marekani kwa matibabu.

Nyarandu amesema kuwa ndege hiyo imewasili salama katika mji wa Charlotte NC nchini Marekani na majeruhi hao wamepelekwa Hospitali ili kuimarishwa afya zao.

Mbunge ameendelea kusema kuwa baada ya kuwasili watachukuliwa na ndege nyingine maalum na kupelekwa hospitali ya Mercy iliyopo Sioux City jimbo la Iowa kwaajili ya huduma ya matibabu kamili.

Watoto hao watatu walinusurika kwenye ajali ya basi iliyoua wanafunzi wenzao 33, walimu wawili na dereva wa shule ya Lucky Vicent ya Arusha wiki iliyopita.

Wanafunzi hao waliondoka jana na ndege aina ya Samaritan’s Purse DC 8 N782SP ambayo iliwasili katika uwanja wa ndege wa KIA uliopo mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya safari hiyo.

 Katika safari hiyo wanafunzi hao waliambatana na wazazi wao kwa ajili ya kuwa nao karibu wakati wa matibabu nchini Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *