Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amewataka askari na Maafisa wa jeshi la Polisi nchini kutotumia madaraka yao vibaya kwa kuwabambikizia wananchi kesi.

Mwigulu Nchemba amesema hayo wakati akifungua kikao cha kazi cha Siku tatu cha mwaka 2017 kwa maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa LAPF Mjini Dodoma.

Mwigulu amesema kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kuwabambikizia kesi, Kuwabadilishia watu kesi zao za msingi kwa sababu ya kushindwa kutoa rushwa hivyo kikao hicho kinapaswa kuwa na maamuzi na maadhimio yenye dira na taswira njema kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Pia amesisitiza pia Askari na Maafisa wa Polisi kutotumia taarifa za watu wanaohasiana kuwa ndio chanzo pekee cha msingi wa shtaka badala yake kufanya uchunguzi kwa kina na kujiridhisha vyema ili kufikia hukumu yenye tija.

Waziri huyo amesema kuwa kufanya hivyo kutaimarisha amani na jeshi la Polisi kupata taarifa nyingi za uhalifu kutoka kwa wananchi endapo watajikita katika haki.

Nchemba amesisitiza pia Jeshi la Polisi kuendelea kupambana na kubaini uhalifu sambamba na kushirikiana na vyombo vingine ili kuhakikisha lengo mahususi la serikali ambalo ni kuzuia uhalifu linafanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *