Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini, Mwigulu Nchemba ametoa tamko rasmi juu ya kitendo cha kupigwa kwa  mwanafunzi wa kidato cha tatu, Sebastian Chinguku wa shule ya sekondari Mbeya Day, na walimu watatu waliokuwa mafunzoni shuleni hapo.

Katika akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, Waziri Mwigulu alisema vyombo vya dola vimeagizwa kuwafuatilia walimu hao, Frank Msigwa na John Deo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Sanke Gwamaka kutoka Chuo cha Nyerere Memorial cha Kigamboni Dar.

Katika video iliyopatikana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, walimu hao walionekana wakimpa kipigo kikali mwanafunzi huyo aliyeshidwa kujitetea, huku mwalimu mmoja wa kike, akisikika akiwaomba waache kumuadhibu namna hiyo kijana huyo.

Kwa mujibu wa Waziri Mwigulu, mwalimu huyo anayesikika, amemtaja kwa majina ya E. H kutoka Iringa University ambaye pia ndiye aliyechukua picha hiyo ya video.

Mwigulu alisema chanzo cha hali hiyo ni kuwa Mwalimu Frank alitoa assignment ya somo la kiingereza kwa wanafunzi wa darasa hilo, lakini baadhi ya wanafunzi hao, akiwemo Sebastian hawakufanya zoezi hilo, jambo lililomfanya mwalimu huyo ampige kibao mwanafunzi huyo, ambaye alihoji sababu ya kupigwa kofi.

Hali hiyo ikasababisha wawili hao kukabana koo, kitendo kilichowafanya walimu wengine kumchukua kijana huyo na kwenda naye ofisini, ambako walianza kumshambulia kwa pamoja wakimpiga kila sehemu.

Wakati uongozi wa shule ya Mbeya Day ukiendelea kuhojiwa na Polisi, Jeshi hilo limetakiwa kuwasaka walimu hao katika vyuo vyao, huku mwanafunzi Sebastian akipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *