Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha Tamasha la Michezo la Karatu litakalofanyika Jumamosi Desemba 17 mwaka huu.

Mratibu wa tamasha hilo, ambaye ni mwanariadha wa zamani na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Riadha Tanzania (RT), Meta Petro amesema mjini hapa kuwa, Waziri Nape ndiye atakuwa mgeni rasmi katika hitimisho la tamasha hilo, ambalo hufanyika kila mwaka.

Mbali na mbio za kilometa 10 kwa wanawake na wanaume, tamasha hilo pia limekuwa likishirikisha michezo ya mbio za baiskeli za kilometa 60, mbio za watoto za kilometa 2.5 na michezo ya mpira wa wavu na soka, ngoma za utamaduni, sarakasi pamoja na kwaya.

Kwa mujibu wa Petro, mchezo wa mpira wa wavu na soka, fainali zake zitafanyika Desemba 16, lakini washindi watakabidhiwa zawadi zao pamoja na wenzao wa riadha na baiskeli Jumamosi Desemba 17 siku ya kilele cha tamasha hilo, ambalo hudhaminiwa na Olympic Solidarity.

Msisimko mkubwa unatarajiwa kuibuka katika mbio za kilometa 10 kwa wanawake na wanaume pamoja na zile za baiskeli, ambazo washiriki wake wengi wanatoka mjini Arusha na maeneo mengine ya Karatu, Mto wa Mbu, Manyara na kwingineko.

.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *