Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ameongoza waombolezaji kumuaga aliyekuwa mpiga picha wa kampuni ya The Guardian, Mpoki Bukuku.

Nape amesema ameondoka bado yapo mambo mengi makubwa, ambayo waandishi nchini wanaweza kujifunza na kuyaendeleza kutokana na kazi zake.

Waziri huyo amesema hayo alipotoa salamu za rambirambi Dar es Salaam jana, alipowaongoza mamia ya waandishi kumuaga Bukuku katika Shule ya Sekondari Tabata iliyopo Kimanga.

Waziri Nnauye amesema yeye binafsi amemfahamu Mpoki siku nyingi kama rafiki, kaka na ndugu wa karibu; na kwamba kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa familia, ndugu na tasnia ya habari kwa jumla.

Kwa upande wake kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema anatoa pole kwa familia, ndugu na waandishi wa habari kwa msiba huo mkubwa.

Mbowe amesema Mpoki ameondoka baada ya kukamilisha wajibu wake kwa familia yake na Taifa; na katika maisha yake alijitahidi mno kujenga jamii na urafiki kwa watu wengi.

Pia amesema waandishi wana wajibu mkubwa kwa Taifa kwa kusema ukweli, kukosoa pale panapostahili na kuwa jasiri, mambo ambayo Mpoki aliyafanya.

Mwisho Mbowe ameomba familia na waandishi wa habari nchini kuwa jasiri na kuwa na moyo wa subira katika kukabili pengo aliloacha mpigapicha huyo maarufu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *