Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba amewataka wananchi wa Kibiti mkoani Pwani kutowaficha wahalifu wanaofanya mauaji mkoani humo.
Mwigulu amewataka wananchi hao wawafichue wahalifu ili maisha yaweze kuendelea kama zamani kabla ya mauaji hayo.
Waziri huyo amewataka wananchi kutambua kwamba kuendelea kuwaficha wahalifu waliopo ndani ya jamii watambue kuna gharama kubwa ambayo itawafanya maisha yasiweze kusonga mbele.
Mwigulu ameyasema hayo jana Kata ya Bungu wilaya ya Kibiti mkoa wa Pwani mara baada ya kutembelea majeruhi na kambi maalum ya jeshi la Polisi mkoani humo.
Pia amesema kwamba serikali imejipanga vyema kubana mianya ya wote wanaofanya mauaji hayo na kuongeza kwamba itawatia nguvuni.
Ameongeza kwa kusema kuwa uhalifu unaoendelea kwa sasa maeneo hayo ya Kibiti yanasababisha wasiwasi kwa wananchi na kuongeza kuwa serikali haitawaacha wahalifu waendelee kufanya mauaji hayo.
Mwisho amemalizia kwa kusema kuwa serikali imeanza kuwabaini wahusika wa vitendo hivyo na bado wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wahalifu wengine.