Jeshi la Polisi limetakiwa kutenda haki kwa wananchi wake na si kuwaongoza watu kama wanyama.

Agizo hilo limetolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa ngazi za juu wa jeshi hilo, yanayotolewa na Chuo cha Aalto Executive Education Academy (AEE) cha nchini Finland.

Mwigulu alisema polisi ni mojawapo ya taasisi inayolaumiwa na kwamba licha ya kuwa kuna mambo mengine mazuri wanayafanya, lakini jamii haiyasifii.

Alisema upungufu huo unasababishwa na kutokuwa na weledi na ujuzi wa kutosha katika uongozi.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema viongozi wote wanatakiwa kupewa elimu ya uongozi ikiwamo ya kuwaandaa viongozi wengine.

Alisema analo jukumu la kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa weledi na maadili.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema karne ya sasa inahitaji viongozi wenye uwezo mkubwa kwa sababu jamii imeelimika zaidi kuliko zamani.

Amesema mabadiliko hayo kwa jamii yamesababisha changamoto za kukithiri kwa uhalifu na kusema kuwa nchi hazina mipaka ya asili kama zamani hali inayosababisha ugumu wa kuwatawala watu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *