Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi amesema wanashukuru kwa kumaliza mzunguko wa kwanza kwa ushindi wenye matumaini ya kurudi katika nafasi yao.

Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara juzi uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Ushindi huo unaipa nafasi Yanga kuweka matumaini yake ya kutetea taji la ubingwa kwa kufikisha pointi 33, akitofautiana kwa pointi mbili na kinara wa ligi wekundu wa Msimbazi, Simba wenye pointi 35.

Mwambusi amesema mchezo wa mwisho ulikuwa ni migumu, lakini muhimu kwao ilikuwa ni kupata pointi na hilo lilifanikiwa.

Mwambusi alisema sasa wanaangalia namna ya kujipanga kwa mzunguko wa pili kwa kuhakikisha wanarudi na kasi waliyomaliza nayo na kulitetea taji lao.

Kwa upande wake, Kocha wa Ruvu Shooting Seleman Mpungwe alisema walijipanga kushinda kwa mbinu zote, lakini ilishindikana baada ya Yanga kuonesha ugumu kwa kuwashambulia na kutumia makosa yao kuwafunga.

Amesema kupoteza katika mchezo huo haimaanishi kuwa timu yake ina mapungufu, isipokuwa kilichotokea ni sehemu ya mchezo na kuahidi kuyafanyia kazi kasoro zao ili kufanya vizuri michezo ijayo ya mzunguko wa pili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *