Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Elimu, Joseph Mungai unatarajiwa kuagwa  leo jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Karimjee.

Mtoto wa marehemu, William Mungai amesema ibada ya kuuaga mwili huo itafanyika katika viwanja hivyo saa 5.00 asubuhi.

Hata hivyo mtoto huyo wa marehemu hakutaka kuingia kwa undani kuhusu chanzo cha kifo cha baba yake, badala yake alisema familia iachwe iendelee kushauriana na daktari.

Amesema pamoja na hayo, kifo hicho kimewashtua kwa vile  kimetokea ghafla na kwamba baada ya kuisha kwa ibada ya kuaga mwili huo, utasafirishwa hadi Mafinga, Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa kwa mazishi.

Kifo cha Mungai kilitokea juzi jioni katika kile kilichoelezwa kuwa   alianza kujisikia vibaya baada ya kunywa kiywaji katika   hoteli moja iliyopo Msasani, ambayo aliizoea.

Mmoja wa waombelezaji waliofika nyumbani kwa marehemu jana ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)- Zanzibar, Salum Mwalimu ambaye alimwelezea Mungai kuwa aliunga mkono  mabadiliko ya siasa.

Mbunge wa zamani wa Kwela, Chrisant Mzindakaya alisema amesikitishwa na kifo hicho ikizingatiwa wiki iliyopita walikuwa pamoja na walizungumza mambo mengi ya siasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *