Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala ameshauri chuo hicho kuangalia uwezekano wa kufundisha baadhi ya masomo kwa lugha ya Kiswahili.

Aliyasema hayo jana chuoni hapo wakati wa hafla ya kutunukiwa kwake Tuzo ya Kiswahili, iliyotolewa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), kwa kutambua mchango wake katika kukuza lugha hiyo na kuifanya kuwa lugha rasmi ya mawasiliano chuoni na katika vikao vya baraza la chuo hicho.

Profesa Mukandala amesema inawezekana kabisa kukawa na masomo yanayofundishwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuikuza lugha hiyo.

Pia amesema tatizo lililokuwa huku nyuma ni kwamba ilipotokea kuna mkutano mikubwa inayowashirikisha wageni wasiojua lugha ya Kiswahili, walitumia Kiingereza katika mikutano hiyo na kwamba, chuo hicho kinaweza sasa kutayarisha vifaa ma mitambo ili wakalimani wavitumie kuwatafsiria wageni hao ili lugha ya Kiswahili iendelee kutumika badala ya Kiingereza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mshiriki wa Tataki, Dk Musa Hans alisema matumizi ya lugha ya kiswahili chuoni hapo ni makubwa na kila leo lugha hiyo inaimarika na kuwa na misamiati mingi na imekuwa ikutumika kama lugha ya mawasiliano, kufundishia na matumizi yasiyo rasmi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *