Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe amemtaka Rais wa Marekani, Donald Trump atambue kuwa hakuna nchi ambayo ina haki ya kumiliki silaha za nyuklia peke yake na kuzuia nchi nyingine kumiliki silaha hizo.

Mugabe ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kuwasili kutoka jijini New York nchini Marekani alikoenda kushiriki mkutano wa 72 wa Umoja wa Mataifa, akijibu kauli ya Trump kuwa ataiharibu kabisa Korea Kaskazini.

Akizungumza Jumatatu katika hafla ya kumkaribisha iliyoandaliwa na chama chake cha Zanu-PF, Mugabe alisisitiza kuwa hakuna nchi ambayo ina haki ya kuionea nchi nyingine na kwamba hakuna nchi ndogo zaidi kijeshi.

“Kila nchi ina nguvu ya kujitawala, bila kujali ni ndogo kiasi gani. Hakuna nchi ambayo ni ndogo kupitiliza. Kwahiyo, tunamuonya [Trump],” Mugabe anakaririwa na gazeti la Serikali la Herald.

Awali, akiwa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa, Mugabe alimtaka Trump ambaye alimtaja kama ‘Goliati’ wa karne hii anayetishia kusambaratisha nchi nyingine, kuendeleza utamaduni wa Jumuiya hiyo wa kuhubiri amani, mshikamano na mazungumzo badala ya vita.

Trump aliionya Korea Kaskazini kuwa ataiharibu kabisa kama atalazimika kufanya hivyo endapo haitasitisha mpango wake wa majaribio ya mabomu ya nyuklia.

Korea Kaskazini imejibu kwa kueleza kuwa kauli hiyo ni dhahiri kuwa Marekani imetangaza vita kamili. Hata hivyo, jana Ikulu ya Marekani ilikanusha madai hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *