Mkazi wa Machimbo Yombo jijini Dar es Salaam, Salum Njwele (34) maarufu kama Scorpion, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kumtoboa macho yote mawili Said Ally.

Scorpion alifikishwa mahakamani jana mbele ya Hakimu Mkazi, Adelf Sachore na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Munde Kalombola.

Kalombola amedai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu eneo la Buguruni Sheli wilaya ya Ilala.

Kolombora amedai kuwa Njwele aliiba mkufu rangi ya fedha wenye uzito wa gramu 34 ikiwa na thamani ya Sh 60,000, bangili na fedha taslimu Sh 331,000 vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya Sh 476,000 mali ya Said Ally.

Kalombola amedai kuwa mshitakiwa kabla na baada ya wizi huo, alimchoma kisu machoni, tumboni na mabegani mlalamikaji ili ajipatie mali hizo.

mtoboa-macho-768x432

Hata hivyo, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na upande wa mashitaka uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutaja.

Hakimu Sachore aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 19, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Mshitakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashitaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *