Tume ya mishahara na marupurupu ya watumishi wa umma nchini Kenya imetangaza kupunguzwa kwa mishahara ya maafisa wakuu wakiwemo rais na wabunge.

Mwenyekiti wa tume hiyo Bi Sarah Serem ametoa mpangilio mpya wa malipo ambao anasema utaokoa jumla ya Sh8 bilioni (dola 80 milioni za Marekani) kila mwaka na kupunguza jumla ya mishahara inayolipwa watumishi wa umma kwa asilimia 35 .

Tume hiyo imependekeza kufutiliwa mbali kwa marupurupu ya kipimo cha usafiri wa magari kwa magavana na wabunge na badala yake hilo litakuwa likifidiwa na mfumo mpya wa marupurupu kwa kuzingatia kanda.

Rais sasa atakuwa akilipwa Sh1.4 milioni kila mwezi badala ya Sh1.5milioni, naye naibu wake awe akilipwa Sh1.2 milioni.

Mawaziri watakuwa wakilipwa Sh924,000, Spika wa Bunge Sh1.1milioni nao magavana wa kaunti Sh924,000.

Bi Serem amesema maafisa wa serikali walikuwa wakitumia vibaya mfumo wa marupurupu wa kupimiwa usafiri wa magari.

Badala yake, maafisa sasa watakuwa wakilipwa marupurupu ya kila mwezi ya usafiri kwa kutegemea eneo anamotoka afisa husika.

Wabunge, ambao wamekuwa wakilipwa marupurupu kwa kuhudhuria vikao vya kamati mbalimbali, pia watakosa marupurupu hayo.

Viongozi wa serikali ya upinzani bungeni, ambao pia walikuwa wakipokea marupurupu ya majukumu maalum pia hawatalipwa tena marupurupu hayo.

Mishahara hiyo mipya itaanza kutekelezwa baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti.

Maafisa ambao mihula yao haitakuwa imemalizika mwaka huu wataendelea kupokea mishahara yao ya awali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *