Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa, Dk. Augustine Lyatonga Mrema amemtaka Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa kuwatoa wafungwa 43 aliowalipia Sh. 12,840,000 walizokuwa wakidaiwa kupitia mfadhili wake Mchungaji Getrude Lwakatare.

Mrema ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wanahabari kwamba ameamua kumwandikia barua Majaliwa ili waliokwamisha zoezi hilo wachukuliwe hatua.

Mrema amesisitiza kwamba azima ya kuwatoa wafungwa magerezani ilikuja baada ya Majaliwa kutembelea Gereza Kuu la Isanga na kukuta msongamano mkubwa wa wafungwa, na katika magereza sita aliyotembelea idadi ilizidi kwa asilimia 16 ambapo palitakiwa kuwa wafungwa 1,552 lakini wakawepo 1,795.

Ameeleza kuwa baada ya mchakato wote kukamilika Oktoba 21 mwaka huu fedha za kuwatoa wafungwa hao zililipwa katika benki lakini akasikitishwa kwamba licha ya wafungwa hao kulipiwa hadi sasa hawajatolewa.

Vile vile Mrema ameongeza kuwa mbali ya kutopewa sababu zozote kwa maandishi zinazokwamisha wafungwa waliolipiwa faini wasiachiwe, anasikia tetesi kupitia vyombo vya habari kwamba zoezi hilo limesitishwa na Jeshi la Magereza.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *