Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda, Diane Rwigara, mamake na dada yake wamefikishwa mahakamani mjini Kigali kwa mara ya kwanza kwa kosa uasi.

Watatu hao wameshitakiwa kuchochea uasi nchini, mashtaka wanayokanusha wakisema yana misingi ya kisiasa.

Diane Rwigara alizuiwa kugombea kiti cha urais katika uchaguzi uliofanyika mwezi wa 8 mwaka huu ambapo Rais Paul Kagame alishinda kwa asilimia 98 ya kura.

Wakati wa kesi hiyo chumba cha mahakama kilikuwa kimejaa watu wengi miongoni mwao wanadiplomasia wa baadhi ya nchi za Magharibi na Marekani.

Ulinzi ukiwa umeimarishwa, watuhumiwa hao watatu waliingizwa mmoja baada ya mwingine katika chumba cha mahakama huku wakifungwa pingu.

Jaji alifungua kikao kwa kusikiliza hoja ya watuhumiwa, Diane Rwigara na Mamake Adeline Rwigara wamesema wana tatizo la kuwasiliana na mawakili wao.

Wamesema wameweza kuwasiliana mara moja tu kabla ya mawakili kukataliwa kuwaona tena huku Dadake Anne Rwigara yeye akisema kuwa hajapa wakili.

Mashitaka yanayowakabili yalikuwa tayari yamewekwa hadharani na mwendeshamashtaka kabla ya wao kufikishwa mahakamani leo.Wote watatu wameshitakiwa kuchochea uasi miongoni mwa wananchi.

Zaidi ya hayo, Diane Rwigara ameshtakiwa kughushi nyaraka huku Mamake Adeilne Rwigara akishtakiwa pia kosa la kugawa wananchi kwa misingi ya kikabila.

Awali walipokuwa katika ngazi ya upelelezi wa mwanzo walishitakiwa makosa ya kutaka kuiangusha serikali na ulaghai wa kukwepa kulipa kodi, lakini makosa hayo yalifutwa.

Wote wanapinga mashitaka dhidi yao wakisema yana misingi ya kisiasa.Diane Rwigara mwenye umri wa miaka 35 alizuiliwa kugombea kiti cha urais uliofanyika mwezi wa 8 mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *