Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho amesema kuwa Liverpool ni timu ya kawaida sana tofauti na vyombo vya habari vinavyoipamba timu hiyo.

Jose Mourinho amesema Liverpool, sio ‘Ajabu la mwisho duniani’ kama vyombo vya habari vinavyoipamba timu hiyo, kauli ambayo ameitoa baada ya Manchester United kutoa sare ya 0-0 na klabu hiyo jana usiku.

Katika mchezo wao huo wa Ligi Kuu ya Uingereza kwenye dimba la Anfield, ulikuwa na nafasi chache za mashambulizi, huku wenyeji Liverpool wakidhibitiwa na safu imara ya ulinzi ya Manchester United iliyocheza kwa nidhamu.

Kocha Jose Mourinho amejigamba kuwa Manchester United imeacha ujumbe wa kumbukumbu ya kuizuia Liverpool kupata ushindi ambao ungewapa pointi tatu wakiwa nyumbani kwao. Katika mchezo huo kipa David de Gea aliibuka shujaa kwa kuokoa magoli.

Kwa upande wake kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema hakufurahishwa namna kikosi chake kilivyocheza, na kusema kuwa walijaribu kucheza haraka lakini walikosa uvumilivu wa pasi zao.

Kwa matokeo hayo Liverpool ipo katika nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza ikiwa na pointi 17, huku United ikiwa pointi tatu nyuma, katika nafasi ya saba ya ligi hiyo ambayo inaongozwa na Manchester City.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *