Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho amesema klabu hiyo inahitaji kusaini mchezaji mwengine kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu nchini Uingereza lakini amekataa kuthibitisha kama wanamuwinda Paul Pogba kutoka Juventus.

Kocha huyo amesema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Shanghai nchini China walipokwenda kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu nchini Uingereza.

Mourinho alipoulizwa kuhusu suala la kutaka kumsajili Paul Pogba amesema hana ruhusa ya kumzungumzia mchezaji wa timu nyingine na Pogba ni mchezaji wa Juventus kwa hiyo awezi kuzungumzia hilo.

Kocha huyo amesema kwamba bodi yake na wakurugenzi wanafanya kazi kwa asilimia 75 kwa hiyo suala zima la usajili anawaachia wao lakini anadhani watafanya usajili mzuri kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Agosti 31 mwaka huu.

Jana vyombo vya habari nchini Uingereza viliripoti kwamba mtendaji mkuu wa Manchester United, Ed Woodward ameikacha safari ya China kwa ajili ya kukutana na kukubaliana na wakala wa mchezaji ,Paul Pogba, Mino Raiola kwa ajili kumsajili mchezaji huyo.

Manchester United tayari imeshasajili wachezaji watatu hadi sasa kwa ajili ya kuimalisha kikosi hiko ambacho kinakabiliwa na michuano tofauti ndani ya Uingereza na nje ya Uingereza.

Wachezaji hao waliosajiliwa na Manchester United msimu huu ni Zlatan Ibrahimovic kutoka klabu za Paris-Saint Germain, Henrikh Mikitharyan kutoka Borussia Dortmund na Eric Bailly kutoka Villareal.

 

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *