Maeneo ya jimbo la California ambayo hukuza mizabibu yameathiriwa na moto mkubwa ambao unaenea kwa kasi sana na kusababisha vifo vya watu 10.

Mamia ya watu wamehamishwa makwao na inakadiriwa kwamba zaidi ya nyumba 1,500 zimeharibiwa na moto huo.

Watu saba waliuawa katika wilaya ya Sonoma, maafisa wamesema.
Watu zaidi ya 20,000 wamekimbia wilaya za Napa, Sonoma na Yuba baada ya moto mbaya zaidi wa nyika kuzuka maeneo hayo.

Kando na watu waliofariki Sonoma, wengine wawili wamefariki Napa na mwingine mmoja Mendocino.

Inaarifiwa kwamba kuna majeruhi wengine zaidi na wapo pia watu ambao bado hawajulikani waliko.

Marian Williams mkazi wa Kenwood, Sonoma amesema yeye na majirani zake waliutoroka moto huo kwa msafara wa magari.

Mkuu wa kukabiliana na moto wilaya ya Napa amesema hali ya kiangazi katika eneo hilo inaathiri juhudi za kuukabili moto huo na kwamba wameomba usaidizi kutoka wilaya nyingine jirani.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imetoa tahadhari eneo lote la San Francisco na kusema “moto ukizuka basi kuna uwezekano utaenea kwa kasi sana”.
Kwa Picha: Moto mkubwa California
Mmiliki mmoja wa mizabibu aliambia gazeti la LA Times kwamba anaamini shamba lake limeharibiwa baada yake na familia yake kukimbilia usalama Jumapili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *