Shirikisho la Soka la Morocco limetangaza kwamba litawasilisha ombi la kutaka kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la 2026.

Siku ya mwisho kwa nchi kuwasilisha nia ya kuwa mwenyeji wa michuano hiyo ni leo Ijumaa, na baadaye Fifa itathibitisha nchi ambazo zimewasilisha maombi.

Marekani, Canada na Mexico zilitangaza mwezi Aprili kwamba zitawasilisha ombi la kuwa wenyeji kwa pamoja.

Ni taifa moja pekee ambalo limewahi kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia barani Afrika – Afrika Kusini mwaka 2010 – na hii itakuwa mara ya tano kwa Morocco kutaka kuwa mwenyeji.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) liliunga mkono juhudi za Morocco mwezi Julai.

Jumla ya timu 48, badala ya 32 ilivyo sasa, zitashiriki katika michuano hiyo mwaka 2026 baada ya timu kuongezwa kwenye mabadiliko yaliyotangazwa na Fifa mapema mwaka huu.

Sera ya Fifa ya mzunguko ina maana kwamba Afrika ni moja ya mashirikisho ambayo yanaweza kuwasilisha maombi ya kuwa mwenyeji wa fainali za 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *