Bingwa wa riadha wa Uingereza, Mo Farah ameaga riadha za uwanjani kwa ushindi katika mbio zenye ushindani mkali za 5,000m za Diamond League mjini Zurich.

Farah mwenye umri wa miaka 34, ambaye ameshinda mataji manne ya Olimpiki, sasa ataangazia mbio za nje ya uwanja.

Alikabiliwa na ushindani mkali sana mita 100 za mwisho na bingwa mpya wa dunia kutoka Ethiopia Muktar Edris lakinia akashinda kwa muda wa dakika 13 na sekunde 06.05.

Mmarekani Paul Chelimo alimaliza wa pili baada ya Edris, aliyemshinda Farah katika mbio za London 2017, kuanguka akipiga mbizi kujaribu kuvuka mstari wa mwisho.

Farah alishinda dhahabu katika mbio za 10,000m katika mashindano ya ubingwa wa dunia wa riadha duniani mwezi huu kabla ya kupoteza taji lake la mbio za 5,000m katika mashindano hayo.

Hata hivyo, alishinda mbio zake za mwisho uwanjani akiwa Uingereza zilizofanyika mjini Birmingham.

Mbio za 5,000m zilikuwa miongoni mwa mataji 16 ya Diamond League yanayoshindaniwa Zurich.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *