Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ametangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Mfanyabiashara Bora wa Afrika wa mwaka 2016 jijini Paris nchini Ufaransa.

Tuzo hiyo imetolewa na kampeni ya Ujasiriamali la Ufaransa (MEDEF), ambalo liliandaa jukwaa la kwanza la vijana na ujasiriamali Afrika kwa kushirikiana na Taasisi ya Choiseul.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Dar es Salaam jana na ofisi ya Dewji, ilisema jukwaa hilo lilimpa tuzo mfanyabiashara huyo kwa kuheshimu mchango wake wa kuleta mabadiliko chanya katika kuendesha biashara, ambayo ni mfano kwa maendeleo na mafanikio ya Afrika katika kizazi cha sasa.

Ikiwa imeanzishwa mwaka 1988, MEDEF ni shirikisho mwajiri mkubwa zaidi nchini Ufaransa, likiwa na wanachama kama vile kampuni kubwa za Total, BNP Paribas, AXA Group, Micheln na L’Oreal.

Dewji ambaye ni Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni za MeTL amezungumza kwa kirefu namna alivyopanga kusaidia mahitaji ya bara la Afrika kupitia maendeleo yanayochagizwa na sekta binafsi.

Dewji ameitaka Ufaransa kuanza kuyatazama kwa mtazamo wa usawa mataifa yasiyozungumza Kifaransa kama ya Afrika Mashariki katika uwekezaji kutokana na ukuaji wa haraka wa uchumi na utulivu wa kisiasa eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *