Mkuu wa Shule ya Sekondari Shinyanga Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Marxon Paul amevuliwa madaraka kutokana na tabia ya ulevi na kushindwa kusimamia taaluma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga amechukua hatua hiyo baada ya kufika shuleni hapo na kukuta mgomo uliochangiwa na tabia ya mkuu huyo.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari katika Halmashauri hiyo, Paul Kasanda amesema mkuu huyo wa shule ameshindwa kuwasimamia walimu anaowaongoza.

Kasanda alisema kutokana na kushindwa kuwasimamia walimu wamekuwa wakijiamulia wenyewe mambo yao na hivyo kutofundisha ipasavyo, hali iliyochangia kuporomoka kwa taaluma shuleni hapo.

Amebainisha kuwa, shule hiyo ambayo ni ya wavulana ya bweni imekuwa ikiporomoka siku hadi siku kutokana na kuwa na uongozi ambao haufanyi kazi yake ipasavyo.

Kwa sasa shule hiyo inaongozwa na Makamu Mkuu, Marco Badalaha hadi pale uteuzi mwingine kuziba nafasi hiyo utakapofanywa na Katibu Tawala wa Mkoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *