Mkuu wa majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa vyombo vya Ulinzi na usalama vinakabiliana na matukio ya uhalifu yanayotokea nchini kadili yanavyojitokeza.

Mabeyo amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kudai kuwa kwa sasa wanataka kujiridhisha kuwa silaha hizo zinazotumika na hao wahalifu zinatoka wapi na watu hao wasiojulikana ni watu wa aina gani, hivyo amewataka wananchi kuviachia vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi yake.

Mabeyo amesema kuwa “Haya matukio tunaendelea kukabiliana nayo kama yale matukio ya Kibiti, kwanini matukio ya Kibiti hayaleti mshtuko mkubwa sana sasa wakati watu waliothirika ni wengi zaidi kuliko matukio ya sasa?

Katika hatua nyingine,Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Venance Mabeyo ametoa tahadhari kwa wananchi kwamba kuna matapeli wanaojifanya wanaajiri vijana kujiunga na jeshi.

Amesema watu hao wanadai fedha ili kuwasajili vijana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jambo ambalo ni kinyume na taratibu za jeshi kuajiri vijana kwa JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Mabeyo ameonya kwamba mtu yeyote atakayetapeliwa na watu hao basi naye atahesabika kama mmoja wa watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na kuchukuliwa hatua mara moja.

Mkuu huyo wa majeshi amebainisha njia mbalimbali ambazo wanazitumia kuajiri vijana jeshini kuwa ni kuwachukua wale waliopitia mafunzo ya JKT au pale wanapotaka watu wenye taaluma adimu kama vile madaktari, wahandisi au wanasheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *