Aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Uhasibu (IAA) cha Njiro mkoani Arusha, Profesa Johannes Monyo amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh milioni 1.5 baada ya kukutwa na kosa la kutoa ajira kwa Chacha Wambura kinyume cha sheria za utumishi wa umma.

Hukumu hiyo ilitolewa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Agustino Rwezile.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimju Mfawidhi Rwezile alisema mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na makosa sita ambapo kosa la 1, 2, 3, 4 na 6 shitaka la ukiukwaji wa taratibu za utumishi wa umma kinyume cha kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Rwezile alisema kosa la 1, 2, 3, 4 mahakama imeona mshitakiwa hana hatia, lakini kosa la tano mshitakiwa aliloshitakiwa nalo la kutoa taarifa za uongo katika Bodi ya Chuo cha Uhasibu Njiro (IAA) ili kumpatia ajira Chacha Wambura, mahakama imemtia nalo hatiani.

Amesema mshitakiwa alitoa tangazo la ajira bila kusubiri majibu ya kibali cha Utumishi na akaendelea kutoa ajira wakati hana mamlaka ya kufanya hivyo na kusababisha Wambura kumpatia manufaa hivyo mahakama imemtia hatiani.

Katika kesi hiyo mshitakiwa alikuwa akishitakiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambao alikuwa akiwakilishwa na Mwanasheria wao, Violet Machary na walileta mashahidi wanne upande wa Jamhuri, huku mshitakiwa akisimama kujitetea mwenyewe.

Baada ya hukumu hiyo mshitakiwa alilipa faini na kujinasua kwenda kutumikia kifungo katika magereza ya Kisongo jijini Arusha.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *