Mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unatarajiwa kuanza leo na kumalizika tarehe 10 Februari 2017 Mjini Dodoma.

Mkutano huo utakuwa ni mahususi kwa ajili ya kupokea Taarifa za mwaka za Kamati za Kudumu za Bunge ambapo Kamati 14 za kisekta na mtambuka zitawasilisha taarifa zake Bungeni katika kipindi hiki.

Kufuatia uteuzi wa wabunge watatu walioteuliwa na Mhe. Rais Dk. John Pombe Magufuli hivi karibuni na Uchaguzi Mdogo uliofanyika katika Jimbo la Dimani, Zanzibar Tarehe 22 Januari 2017, kutakuwa na Kiapo cha Uaminifu kwa Wabunge wapya wanne ambao ni:-

(i)         Mhe. Alhaji Abdallah Majula Bulembo

(ii)       Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi

(iii)      Mhe. Anne Kilango Malecela

(iv)    Mhe. Ali Juma Ali – (Jimbo la Dimani)
 

Katika Mkutano huu jumla ya maswali ya kawaida 125 yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa Bungeni.

Aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya 38 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge wastani wa maswali 16 ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yataulizwa na kujibiwa pia siku za Alhamisi.

Katika Mkutano wa Tano wa Bunge uliomalizika mwezi Novemba, 2016 Miswada mitatu (3) ya Sheria ilisomwa  kwa mara ya Kwanza Bungeni na kupelekwa kwenye Kamati husika ili ifanyiwe kazi.

Hivyo katika Mkutano huu wa Sita Miswada hiyo inatarajiwa kuwasilishwa Bungeni kwa mara ya Pili, kujadiliwa na kupitishwa na Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 91.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *