Mkulima wa kijiji cha Dodoma Isanga kata ya Masanze wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Augustino Mtitu amechomwa mkuki mdomoni na kutokea shingoni.

Mtitu na wengine wanane walijeruhiwa katika vurugu zilizohusisha jamii ya wafugaji wa Kimasai na wakulima wa kijiji hicho kilichopo wilayani Kilosa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alisema mpaka jana watu watatu walikuwa wanashikiliwa na Polisi, na msako unaendelea kuwasaka wale wote waliohusika katika kufanya vurugu hizo.

Tukio hilo ni limetokea Desemba 25, mwaka huu baada ya mtu huyo kujaribu kuzuia vurugu hizo, zilizokuwa zimetokea baada ya wafugaji hao kulisha mifugo yao katika shamba la maharage na mahindi katika kijiji hicho.

Mtitu akijaribu kuzuia vurugu hizo, aliishia kuchomwa mkuki na mmoja wa wafugaji wa jamii hiyo, ambao baada ya tukio hilo walikimbia kutoka eneo hilo.

Kutokana na tukio hilo, wananchi wenzake waliamua kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya matibabu.

Lakini, alihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji na matibabu zaidi ya kuokoa maisha yake.

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, muda mfupi baadaye wafugaji hao walirudi tena kijijini hapo, kwa lengo la kuokoa mifugo yao iliyokuwa imekamatwa, na ndipo walipoanzisha tena vurugu kwa kuwashambulia watu wengi wanane akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji pamoja na wa Kitongoji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *