Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema ana mpango wa kupeleka bungeni maombi ya kuongezwa muda wa kustaafu maprofesa.

Amesema umri wa kustaafu kwa sheria unawafanya wasomi hao washindwe kutumika vizuri kulijenga Taifa, hivyo ataomba wastaafu wakiwa na umri wa miaka 65 badala ya 55.

Mkuchika amesema hayo leo alipotembelea ofisi za Sekretarieti ya Ajira na kukutana na watendaji wa taasisi hiyo.

Amesema baadhi ya kada ambazo zinafanyiwa kazi na maprofesa zinatakiwa kuangaliwa kwa jicho la tofauti.

Waziri amesema wengi wanapata  uprofesa wakiwa na miaka 55 na hufanya kazi kwa miaka michache na kutakiwa kustaafu.

Amesema haitakuwa na maana kama wasomi hao wanatumia rasilimali za Taifa kufikia hatua hiyo halafu baada ya kuhitimu wanafanya kazi kwa muda mfupi na kutakiwa kustaafu.

Mkuchika amesema pia atawasilisha maeneo mengine ambayo yana upungufu unaotokana na sheria.

Kuhusu watumishi wa umma walioshiriki na kushinda katika uchaguzi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema watawashughulikia kulingana na mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi.

Amesema wakati nchi inaingia kwenye mfumo wa vyama vingi, Katibu Mkuu Kiongozi alitoa mwongozo ambao ulielekeza kuwa kuna baadhi ya watumishi wa umma kulingana na nafasi zao wapo wanaoruhusiwa na wasioruhusiwa kushiriki kwenye siasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *