Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa leo ameanza ziara ya kikazi nchini Burundi hadi Desemba 9 akiwa msuluhishi kati ya Warundi huku akitazamiwa kukutana na viongozi mbalimbali serikalini na mashirika ya kiraia.

Ziara hiyo inakuja wakati nchi hiyo bado inakabiliwa na mgogoro huku mazungumzo yakiwa yamesimama kwa miezi kadhaa sasa.

Hata hivyo serikali ya Burundi iliapa kutokaa kwenye meza ya mazungumzo na makundi ya watu ambao inadai kuwa walihusika katika jaribio la kuipindua serikali lililoshindwa Mei 13 hadi 14 mwaka jana.

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Marekani wamekua wakiomba serikali ya Burundi kuanzisha haraka bila masharti mazungumzo na upinzani uliokimbia uhamishoni kwa lengo la kudumisha usalama na kurejesha amani nchini mwake.

Hali ya usalama nchini Burundi imeendelea kutisha katika maeneo mbalimbali, hasa mjini Bujumbura, ambapo maiti kadhaa zimekuwa zikiokotwa huku visa vya utekaji nyara vikikithiri katika baadhi ya maeneo ya nchi ya Burundi.

Machafuko nchini Burundi yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 500 kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu na zaidi ya 250,000 kuyahama makazi yao na kukimbilia nje ya nchi.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *