Mjane aliyelalamika kudhulumiwa mirathi mbele ya Rais John Magufuli, katika sherehe za siku ya Sheria, amefunguliwa kesi na mtoto wa marehemu akidai fidia ya Sh milioni 400 kwa kumtaja kuwa anajihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Kesi hiyo ya madai imefunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na mmoja wa watoto wa Marehemu Shosi, Saburia Shosi dhidi ya mjane wa marehemu, Swabaha Shosi.

Katika kesi hiyo namba 38 ya mwaka 2017, Saburia ambaye anawakilishwa na Wakili Abdon Rwegasira, anaiomba mahakama itamke kuwa tuhuma hizo zilizotolewa na mama huyo dhidi yake ni kashfa, pia imwamuru mama huyo amlipe kiasi hicho cha fedha kama fidia ya madhara aliyoyapa kutokana na kwa kashfa hizo, riba pamoja na gharama za kesi.

Kwa mujibu wa hati ya madai ya kesi hiyo, Saburia anadai kuwa yeye ndiye aliyeteuliwa kuwa msimamizi wa mali za marehemu baba yao, Shosi na kwamba mdaiwa alitoa taarifa hizo kwa nia mbaya kwa lengo la kumdhuru kwa kumharibia jina lake, tabia na mahusiano ya kijamii ndani na nje ya nchi pamoja na hali yake kiuchumi.

“Mdaiwa alitoa taarifa hizi kwa hasira na kwa nia mbaya ya kutaka kupata huruma ya rais kwa jambo ambalo liko katika Mahakama za Kisheria na kwamba matokeo ya taarifa hizo zimesababisha watu waniepuke, maumivu makubwa kimwili, kiakili na kisaikolojia na biashara zangu kuvurugika,” inasema hati yake ya madai.

Source: Mtanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *