Zaidi ya milioni 100 zimetumika kumtibu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu baada ya kushmbuliwa na risasi wiki iliyopita.

Hayo yasemwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Nairobi nchini Kenya akitoa taarifa juu ya afya ya Tundu Lissu aliyelazwa katika hospitali ya Aga Khan nchini humo.

Lissu alishambuliwa kwa risasi zipatazo 32 wakati akiwa kwenye gari lake lililoegeshwa nje ya majengo ya nyumba anayoishi akiwa Dodoma wakati wa shughuli za Bunge.

Risasi tano zilimpata mwilini, lakini akaepuka kifo na kwa sasa amelazwa Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi, ambako hali yake imeelezwa kuwa nzuri.

Mbowe amesema kuwa matibabu yake pia yalihitaji vifaa tiba visivyo na shaka yeyote ili kuokoa maisha yake baada ya “kazi na kubwa na ya kupongezwa ya awali iliyofanywa na madaktari wetu kadhaa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma”.

Mbowe amesema Lissu alitibiwa na madaktari wapatao kumi wa fani tofauti baada ya kufika Nairobi na walifanya kazi hiyo usiku kucha na anaendelea kutibiwa muda wote akiwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu, lakini juzi aliweza kuzungumza.

Pia amesema watu kutoka sehemu mbalimbali wamekuwa wakitaka kumtemebelea, lakini hawaruhusiwi na ulinzi umeimarishwa katika eneo analotibiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *