Meneja wa klabu ya Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema siri ya timu yao kufanya vizuri kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ni ubora wa kikosi walichokisajili pamoja na umoja na mshikamano waliokuwa nao.

Simba ndiyo vinara wa ligi hiyo ikiwa na pointi 20 huku ikiwa ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mchezo hata moja katika mechi nane ilizocheza msimu huu.

Mgosi amesema kuwa ubora waliokuwa nao msimu huu ni vigumu kuwazuia kwa sababu wamekamilika katika idara zote muhimu ambazo ndizo zinachangia wapate matokeo hayo mazuri.

Mkongwe huyo aliyestaafu soka mwanzoni mwa msimu huu na kukabidhiwa cheo hicho cha Umeneja alisema, pamoja na kasi waliyoanza nayo lakini mambo bado kwani malengo yao ni kuhakikisha wanaendelea na kasi hiyo na kuhakikisha wanarudisha furaha kwa mashabiki wao wote wanaoipenda Simba katika kipindi chote ambacho walikaa na majonzi kutokana na timu hiyo kufanya vibaya.

Simba chini ya kocha Joseph Omog, imeshinda mechi sita na kutoka sare mbili, matokeo ambayo yameonesha kuvunja rekodi ya timu hiyo kwa misimu mitatu iliyopita ambapo haikuwa ikianza na kasi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *