Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limemkamata mfanyabiashara maarufu mkoani humo, Steven Samweli maarufu kwa jina la Maranatha kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari amesema kuwa Maranatha alikamatwa juzi usiku akiwa katika moja ya maduka yake ya dawa baridi.

Pamoja na hayo, kamanda huyo wa polisi alisema kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo kunafikisha idadi ya watu wanane waliokamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya mkoani Mbeya.

Kamanda amesema kuwa “Miongoni mwa hawa tunaowashikilia, baadhi yao walikutwa na vielelezo, hivyo watafikishwa mahakamani wakati wowote wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.

Aliongeza kwa kusema kuwa “Kwa hiyo, nawaomba wananchi mkoani hapa, waachane kabisa na biashara ya dawa hizo kwa sababu wakikutwa nazo, watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola,”.

Kutiwa nguvuni kwa mfanyabiashara huyo ni mwendelezo wa nia ya Serikali ya kupambana na biashara ya dawa hizo nchini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *