Mwanamke tajiri zaidi barani Afrika Isabel dos Santos, mtoto wa  rais wa Angola amejiongezea utajiri baada ya kununua hisa katika benki kubwa zaidi nchini humo.

Bi Santos amechukua udhibiti wa benki hiyo ya BFA baada ya kampuni yake kununua hisa zaidi katika benki hiyo na kudhibiti zaidi ya asilimia 50 ya hisa katika benki hiyo.

Hatua hiyo imewaacha waangalizi kutojua ikiwa watamshangilia mama huyu mjasiria mali au kulalamikia mamlaka na ushawishi wa kiuchumi walio nao matajiri wachache sana barani afrika.

Isabel dos Santos mwenye umri wa miaka 43, amefanikiwa na angali na ari ya kufanikiwa zaidi katika kanda ambayo wanaume wanatawala katika ofisi nyingi za umma na za kibinafsi.

Bi Dos Santos, ni bintiye rais wa angola Jose Eduardo dos Santos, ambaye ameongoza taifa hilo tangu mwaka 1979.

Katika miaka ya hivi karibuni ilinufaika pakubwa kutokana na mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta na uwekezaji kutoka uchina.

Hata hivyo ufisadi na umaskini vimesalia kuwa changamoto kubwa zaidi nchini humo.

Bi Dos Santos mara kwa mara amepuuzilia mbali madai kuwa familia ya rais inapewa nafasi zaidi kuliko raia wengine kuthibiti uchumi na masuala ya kisiasa ili kuhakikisha kuwa familia hiyo itaendelea kutawala Angola baada ya rais Dos Santos kustaafu, kama alivyohaidi hivi majuzi.

Kwa sasa Bi Dos Santos anasimamia shirika la mafuta la taifa na kampuni kubwa zaidi ya kutoa huduma za simu na sasa anadhibiti benki kubwa zaidi nchini Angola BFA.

Hii ikiashiria kuwa ushawishi wa familia ya rais dos santos itaendelea kuchukua nafasi kubwa zaidi katika masuala ya kiuchumi na kisiasa nchini Angola miaka zijazo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *