Klabu ya Barcelona imemtangaza Ernesto Valverde kuwa kocha wao mpya, mtu mzima huyo wa umri wa miaka 53 akisaini mkataba wa miaka miwili.

Rais wa klabu, Josep Maria Bartomeu ametangaza uteuzi wa kocha huyo mpya katika mkutano na waandishi wa habari leo, ikiwa ni siku mbili baada ya Luis Enrique, aliyeshinda mataji tisa kati ya 13 ndani ya misimu mitatu kuondoka kwenye klabu hiyo.

Valverde anafuata nyayo za Pep Guardiola, Tito Vilanova na Luis Enrique ambao kwanza walianza kama wachezaji wa klabu hiyo kabla ya kuwa makocha.

Wote walishinda mataji ya Ligi katika misimu yao ya kwanza na jukumu la kwanza la Valverde kuwarejeshea Barcelona taji hilo baada yaa msimu huu kuchukuliwa na Real Madrid.

Atakuwa na muda mfupi sana kabla ya kumenyana na Real Madrid mara tatu – kwanza kwenye ziara ya klabu ya kujiandaa na msimu mpya na baadaye mara mbili kwenye Super Cup ya Hispania nyumbani na ugenini.

Valverde aliichezea Barcelona kwa miaka miwili, kuanzia 1998 hadi 2000 akicheza jumla ya mechi 20 na kufunga mabao manane kama mshambuliaji akishinda mataji ya Kombe la Washindi na Kombe la UEFA, kabla ya kusaini Bilbao ambako alicheza kwa miaka sita.

Uteuzi wake wa sasa unatimiza ndoto za pande zote mbili kufanya kazi pamoja, kwani ndiye aliyekuwa chaguo halisi wakati Tata Martino anaondoka Barcelona mwaka 2014, lakini ghafla Barca ikamgeukia Enrique.

Mwanzoni mwa msimu wakati Enrique alipoiambia bodi ya Barcelona hataongeza mkataba mwishoni mwa msimu, wakamuambia Valverde asiongeze mkataba Athletic Bilbao ili ahamie Nou Camp kiulaini.

Ametua na wasaidizi wake mwenyewe katika benchi la ufundi huku aliyekuwa Msaidizi wa Enrique namba mbili, Juan Carlos Unzue akihamia Celta Vigo na Jon Aspiazu akiwa msaidizi wa Valverde.

Hii si mara ya kwanza kwa Valverde kufanya kazi mjini Barcelona, kwa sababu aliifundisha Espanyol kuanzia mwaka 2006 hadi 2008 ambako aliiwezesha klabu kushika nafasi ya pili kwenye Kombe la UEFA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *