Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo amesema Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob ataendelea kuwa rumande hadi agizo la saa 48 lililotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori litakapokamilika.

Jacob alichukuliwa na polisi juzi saa sita mchana akiwa makao makuu ya manispaa hiyo, Kibamba, akiwa katika msafara uliokuwa unaelekea kukagua miradi ya maendeleo akiwa na viongozi wenzake wa Chadema, akiwamo mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Ingawa polisi hawakusema sababu ya kumhitaji, Kilewo aliliambia gazeti hili kuwa chombo hicho cha dola kiliamua kumweka rumande meya kwa kosa la kutumia ukumbi wa halmashauri kwa shughuli za chama bila mkurugenzi kuwa na taarifa.

Kilewo alidai kosa jingine ni hatua yake ya kutaka kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo akiwa na viongozi wa chama chake ambao si madiwani.

Baada ya Jacob, ambaye ni diwani wa Ubungo kuwekwa rumande, taarifa zilisambaa zikieleza kuwa mkuu wa wilaya ameagiza akamatwe pamoja na viongozi wengine.

Wakili wa meya huyo, Frederick Kihwelo alisema mteja wake yupo katika hali nzuri na kwamba wanasubiri busara za mkuu wa wilaya za kumwachia au kumalizika kwa saa 48 alizozitoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *