Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamealikwa kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais mpya wa Ghana, Nana Akufo-Addo kwenye sherehe zitakazofanyika kesho Januari 7 mwaka huu.

Viongozi waliopata mwaliko huo ni Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa Chama, Dkt. Vincent Mashinji ambao wameondoka nchini usiku wa Januari 6, kuelekea Accra, pia watahudhuria kuapishwa kwa Spika wa Bunge la Ghana, pamoja na Wabunge 275, waliopatikana baada ya Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Mbowe na Katibu Mkuu Dkt. Mashinji wamepewa heshima ya kufanya mazungumzo na Rais Nana Akufo-Addo yatakayofanyika Jumapili ya Januari 8, baada ya kupata chakula cha mchana pamoja.

Kabla ya hapo, mapema asubuhi ya siku hiyo, viongozi wakuu wa CHADEMA watakuwa sehemu ya msafara utakaomsindikiza Rais Nana Akufo-Addo, kwenda kwenye ibada ya asubuhi, itakayofanyika eneo la Kyebi, kisha jioni msafara utarejea jijini Accra kuendelea na ratiba zingine.

Viongozi wengine mashuhuri kutoka Afrika walioalikwa katika sherehe hizo ni pamoja na Kiongozi wa Chama cha Forum for Democtratic Change (FDC), Kizza Besigye, kutoka Uganda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *